Rais Jakaya Kikwete amemwagiza Waziri Mkuu Mizengo Pinda kumuondoa haraka katika kituo cha kazi Mthamini wa Ardhi wa Wilaya ya Bagamoyo, Patrick Cecy, kutokana na kubainika kufanya ‘faulo’ katika ulipaji fidia wananchi waliotoa ardhi yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa mradi wa Bandari ya Bagamoyo.
Wananchi walioondolewa katika vijiji ili kupisha mradi huo ni kutoka Pande, Mlingotini, Zinga na Kilomo.
Alitoa agizo hilo jana wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo inayojengwa wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, mradi ambao utagharimu Dola za Marekani bilioni 10 hadi utakapokamilika.
Alisema wakati harakati za ujenzi wa mradi huo zikiendelea, zipo taarifa za manung’uniko ya wananchi walioanza kulipwa fidia kwamba kiasi walicholipwa ni kidogo kutokana na ujanja uliofanywa na mthamini wa ardhi.
‘Wanalalamika baadhi ya fomu zimenyofolewa, mtu ameandika ana hekta 20 lakini zinakatwa anaandikiwa hekta nane, minazi inaandikiwa 100 analipwa 50,’ alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na wananchi ambao wamedhulumiwa.
Rais Kikwete, alisema hapendi kuona mradi mkubwa wa ujenzi wa bandari unatekelezwa huku watu wakiwa wananung’unika, kwani serikali wakati wote haiwezi kuwaumiza watu maskini.
Nasikia mtathimini ndio mkorofi, Waziri Mkuu mbadilisheni, wathamini wapo wengi katika nchi hii, kwani nchi hii yupo pekee yake, alihoji.
Alisema mtathimini huyo kuanzia leo (jana), atafute pa kwenda na akabidhi ofisi kwani mambo anayoyafanya yanafitinisha wananchi na serikali na kwamba angependa kuona bandari inakamilika kukiwa hakuna manung’uniko ya wananchi.
Rais Kikwete alisema wananchi walihamishwa kupisha mradi huo kwa kuwa kuna makaburi ya ndugu zao, kama itawezekana wawe wanapewa nafasi ya kwenda kuzulu makaburi hayo au yahamishwe.
‘Huyu kijana kama haeleweki na wenzake apelekwe sehemu nyingine ambako ataeleweka lakini hapa haeleweki,’ alisema.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, alisema wananchi walioondolewa katika vijiji hivyo mbali na kulipwa fidia pia serikali itawajengea nyumba za kuishi zitakazojengwa eneo la Kindagoni.
Kati ya wananchi 2041 wanaodai fidia 2011 wameshalipwa hadi sasa na waliobaki serikali inaendelea kuwalipa.
Mradi mzima wa ujenzi utajumuisha eneo la hekta 800 kwa ajili ya ujenzi wa bandari na eneo la hekta 1,700 kwa ajili ya ukanda wa viwanda.
Eneo hilo litaendelezwa chini ya makubaliano ya Serikali ya Tanzania, Kampuni ya China ya Merchants Holdings International (CMHI) na Mfuko wa Taifa wa Dharura wa Oman (SGRF).
Chini ya ushirikiano huo, serikali inawakilishwa na Mamlaka ya Bandari ya Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Oman itawakilishwa na SGRF na China CMHI.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment