Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania, (JWTZ), wanaolinda Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi, wanatuhumiwa kuwatesa na kuwachapa viboko madereva na makondakta wa daladala wanaotumia kituo cha abiria cha Kisonge, mjini hapa.
Malalamiko hayo yamejitokeza siku moja tangu askari hao walipoanza ulinzi katika maeneo nyeti ya huduma za jamii.
Ulinzi huo umeanza siku chache kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Maeneo yanayolindwa na jeshi hilo ni kituo cha matangazo cha televisheni na radio vya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Bandari, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Mnara wa Kumbukumbu wa Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Uwanja wa Michezo wa watoto, Kariakoo.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya madereva na makondakta wa daladala, walisema walianza kukamatwa na kupigwa jana saa 12:50 asubuhi, wakati magari ya abiria yaliposimama kuteremsha abiria katika kituo cha Kisonge, jirani na mnara huo katika mtaa wa Michenzani.
Walisema kila gari iliyosimama katika kituo hicho, abiria walitakiwa kuteremka na kutembea, kumalizia safari zao.
Shuhuda wa tukio hilo, Issa Hassan Shabani, mkazi wa Michenzani alisema, baada ya kuteremshwa dereva na kondakta walibaki na kuanza kuteswa wakitakiwa kuruka kichura na baadae kuchapwa viboko.
Watu walikusanyika kama wanatizama sinema wakati madereva wanachapwa na kupewa adhabu ya kuruka kichura, alisema.
Dereva Ali Hamd Faki, mkaazi wa Kinuni, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, alisema alipofika katika kituo cha abiria cha Kisonge alitakiwa na askari wa JWTZ kuteremka pamoja na kondakta wake na kuulizwa kwanini amesimamisha gari karibu na eneo la mnara.
Tunapigwa na kuteswa bila hatia kama kituo cha abiria Kisonge kimefungwa kwanini serikali imeshindwa kutangaza wananchi tukapata kufahamu, alihoji Faki.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hana taarifa yoyote ya madereva na makondakta kupigwa na askari hao.
Alisema suala la kupanga vituo vya abiria ni jukumu linalosimamiwa na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.
Kama kuna mabadiliko yoyote basi wao ndiyo watakuwa wanafahamu, alisema Waziri Aboud ambaye ni msemaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Hakuna mabadiliko ya vituo yaliyofanyika na suala vituo vya daladala vinaratibiwa na kusimamiwa na baraza la manispaa ndiyo wahusika, alisema Naibu waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Gavu.
Alisema mabadiliko yoyote ya vituo yanapofanyika lazima serikali itangaze kabla ya kuanza kutumika ili kuondosha usumbufu kwa wananchi.
Upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, alisema hawana taarifa yoyote ya kufanyika kwa mabadiliko ya vituo vya Daladala katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Kabla ya JWTZ kuanza kulinda maeneo hayo, yalikuwa yakilindwa na askari wa Kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), ambapo pia huduma za kibenki zimeathirika kwa watu wanaotumia mashine za ATM, zilizowekwa katika mnara huo.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment