Basi la New Force Lapata Ajali na Kuua Watu 12 Iringa MAJINA YA WALIOFARIKI YAJULIKANA TAZAMA HAPA


Watu 12 wamefariki dunia papo hapo baada ya lori la mbao lililokuwa likitokea njombe kwenda jijini Dar es Salaam kupasuka tairi na kugongana na basi la abiria la new force lililokuwa linatokea jijini Dar es Salaam kuelekea tunduma hii leo katika eneo la kitonga wilaya ya kilolo mkoani iringa.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa wa iringa, kamishina msaidizi wa polisi Ramadhani Mungi amesema kuwa waliokufa ni wanaume nane na wanawake wanne majeruhi ni 28 ambao wengine wamepelekwa iringa mjini na wengine wako katika hospitali ya wilaya kilolo-iringa.

Aidha Kamanda Mungi amewataka madereva kuwa makini hasa katika kipindi hiki cha sikukuu na kuepuka mwendo kasi pamoja na kutoa taarifa pale vitendo kama hivyo vinapotokea


BAADA YA Marekani Kupitia Shirika la MCC KUinyima Mabilioni Ya Pesa Tanzania Kutokana na Mzozo wa Uchaguzi ZANZIBAR HAYA NI MENGINE MPYA YALOIBUKA.


Tamko kutoka kwa Balozi Mark B. Childress kuhusu uamuzi wa Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia kuahirisha kupigia kura mkataba wake na Tanzania

 *********

Tarehe 16 Disemba, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) haikuichagua Tanzania kwa mkataba wa pili. Bodi iliahirisha kupigia kura mkataba wa pili, ikisubiri kutatuliwa kwa masuala ya kiutawala.

Bodi inaweza kuangalia upya ustahilifu wa Tanzania mwaka 2016. Ninatumaini kwamba Serikali ya Tanzania itachukua hatua hivi karibuni zitakazotatua masuala hayo ya kiutawala. Halafu, Bodi itaweza kupiga kura kuichagua tena Tanzania na kuidhinisha maendeleo ya mkataba.

Masuala ya kiutawala ya Bodi yanaakisi maadili ya muda mrefu ya MCC. Kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar kulisitisha mchakato wa uchaguzi uliokuwa unaenda vizuri na kwa amani. 

Matumizi ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 kuwakamata watu waliokuwa na kibali halali kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi yalikwaza uhuru wa msingi wa kujieleza na kukutana.

MCC imetiwa moyo na hatua zilizochukuliwa hivi karibuni na Rais Magufuli za kuimarisha vita dhidi ya ubadhilifu na rushwa. MCC inatumaini kuwa jitihada hizo zitaendelea na kuleta mabadiliko ya kimfumo.

Zitto Kabwe Amkingia Kifua Profesa Muhongo kwa Hoja NZITO NA HIKI NDICHO alicho KAZIA

Waliosema Ufisadi ni Mfumo ndio wanasema leo Prof. Muhongo hafai kuwa Waziri sababu ya Tegeta Escrow. Sijui lini mahakama ilimhukumu Muhongo! Sijui lini Muhongo kawa Mfumo. Tujifunze kuweka akiba.

Prof. Sospeter Muhongo alikuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati wa sakata la ‪TegetaEscrow‬. 

 

Kamati ya Bunge ilipendekeza na Bunge kuazimia kuwa Muhongo avuliwe madaraka yake ya Uwaziri. Prof. Muhongo alijiuzulu. 

 

Akafanyiwa uchunguzi na Kamishna wa Maadili kutamka kuwa hakukutwa na kosa la kimaadili. Unajengaje hoja kuwa hana haki ya kuteuliwa kuwa Waziri?

 

 Keshaadhibiwa kwa kosa la awali, kwa kujiuzulu. Sheria ipi inasema hana haki ya kuteuliwa tena?

Niliongoza Kamati ya PAC. Nina uhakika Waziri muhongo kwenye sakata lile alishauriwa vibaya na kujikuta anatetea ubadhirifu. 

 

Lile nifunzo kubwa kwake na ninavyomuona sasa hatarudia tena makosa yale. Kuna mambo ya msingi lazima afanye sasa

1) Azuie kuanzia sasa malipo ya 'capacity charges' kwa kampuni ya kitapeli ya IPTL na atumie sheria kutwaa mitambo ya IPTL na kumilikisha TANESCO

2) Amtake Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kumkamata mara moja anayejiita mmiliki wa IPTL na afunguliwe mashtaka ya utapeli, wizi wa udanganyifu na uhujumu uchumi; huyo mmiliki na washirika wake ambao ni raia wa Tanzania

3) Amtake Gavana wa Benki Kuu na FIU kuichukulia hatua za kisheria Benki ya Stanbic ikiwemo kupiga faini ya kurejesha fedha zote zilizokua kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Hizo ndio hoja za msingi na sio uteuzi wa Prof. Muhongo. Mwenye ushahidi dhidi ya Muhongo si aende Mahakamani? Tuache siasa za porojo porojo

By: Zitto Kabwe

Waziri Wa Ajira Jenista Mhagama AMFUKUZA Kazi Mkandarasi Dar......Atoa Masaa 6 Kwa Mkurugenzi wa Kinondoni

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amemtimua kazi mkandarasi anayejenga mfereji wa Buguruni kwa Mnyamani, Manispaa ya Ilala kwa kushindwa kuujenga kwa kiwango kinachotakiwa.

Mbali ya kuchukua hatua hiyo jana, pia Waziri Mhagama aliagiza mkandarasi huyo asilipwe chochote.

Akiwa Tegeta, waziri huyo alimbana Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Ando Mwankuga na kumpa saa sita ampelekee taarifa ya ujenzi wa mfereji wa Tegeta – Basihaya uliojengwa chini ya kiwango.

Maeneo hayo ni yale ambayo miezi saba iliyopita, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliagiza ijengwe mifereji haraka ili kunusuru uhai wa wananchi waliokuwa wanasumbuliwa na mafuriko ya mara kwa mara.

Machi 24, Kikwete aliagiza kuvunjwa kwa nyumba zilizojengwa juu ya karavati lililoziba na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba za wakazi wa maeneo hayo, agizo ambalo bado halijatekelezwa.

Mvua iliyonyesha siku mbili zilizopita ilisababisha nyumba 200 za eneo la Basihaya - Tegeta kukumbwa na mafuriko na nyingine 500 za eneo la Buguruni kwa Mnyamani zikiwa hatarini.

Mafuriko ya wakati huo yalitokana na mvua zilizonyesha kwa wiki mbili mfululizo na kusababisha vifo vya watu 12 huku mamia wakikosa makazi yao. Kutokana na hali hiyo, Mhagama aliagiza wahandisi waliosimamia mradi wa Basihaya, kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua za kisheria akiwaita ni ‘wahandisi mizigo’.

Akiwa Buguruni kwa Mnyamani, Mhagama alishuhudia ujenzi wa mfereji wa maji ulio chini ya kiwango huku ukiwa haujakamilika. Mfereji huo uliokuwa ukitakiwa kukamilishwa kwa miezi mitatu tangu Mei, ungegharimu Sh300 milioni.

“Huu ni utani wa maisha ya Watanzania. Imepita miezi mingi hapa katikati na jua lilikuwa linawaka. Ina maana mkurugenzi na mkandarasi hamjawahi kuja kuona nini kinaendelea? Naagiza huyu mtu asiendelee kujenga na wala asilipwe hata shilingi mia moja. Kama mlishamlipa, fedha hizo mtaifidia Serikali,” alisema Mhagama.

Aliwatahadharisha kuwa ikiwa mvua zitanyesha na kusababisha maafa kwenye eneo hilo kabla mfereji kukamilika, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Isaya Mungulumi na Mhandisi wake, Jaffari Bwigane watawajibika.

Ikiwa mfereji huo utajengwa kwa uhakika, utasaidia kunusuru watu zaidi ya 1,163 wa eneo hilo, kukumbwa na mafuriko kama kipindi kilichopita.

Katika ufafanuzi wake, Mungulumi alisema walibaini kuwa mkandarasi huyo ameshindwa kujenga kwa kiwango wiki mbili zilizopita na kwamba, tayari walianza kumchukulia hatua.

Aliilalamikia Sheria ya Ununuzi ya Umma kuwa ndiyo iliyowafanya kumpa muda wa wiki mbili ajirekebishe kabla ya kumtimua kama ilivyofanyika. “Bado hatujamlipa kiasi chochote cha fedha kwa sababu mkataba wetu ni ujenzi kwanza, ndipo alipwe,” alisema.

Akiwa Tegeta Basihaya, Mhagama alisema: “Wahandisi mizigo wanaoshindwa kusimamia miradi muhimu kama hii lazima wachukuliwe hatua za kisheria. Wote wavunjaji wa sheria na wanaoshindwa kusimamia sheria hawawezi kuendelea kuwa chanzo cha maafa kwa watu wengine.”

Alimtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Paul Makonda kusimamia suala hilo ili kunusuru maisha ya wananchi kwani nyumba 200 zimezingirwa na maji.

Alisema haiwezekani mvua ya saa chache ikasababisha mafuriko kwenye eneo ambalo tayari Kikwete alishatoa maelekezo.

Kikwete aliagiza Manispaa ya Kinondoni kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye mkondo wa maji katika eneo hilo, agizo ambalo halikutekelezwa. Kutokana na hali hiyo, Mhagama aliagiza zibomolewe.

Makonda alikiri ujenzi huo kutokuwa wa kiwango: “Nashukuru waziri umekuja, ni kweli wapo watendaji mizigo kwenye halmahauri yetu, hasa hawa wasimamizi wa miradi kama hii inayojengwa kuokoa maisha ya wananchi.”

Katika taarifa aliyoitoa kwa Kikwete, Makonda alisema mradi huo ili ukamilike ungehitaji zaidi ya Sh3 bilioni. Jana Diwani wa kata ya Kunduchi, Michael Urio alisema kuwa Sh1.2 bilioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao bado unahatarisha maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Kaimu Mkurugenzi, Mwankunga alisema upungufu uliojitokeza kwenye mradi huo utarekebishwa. “Kabla ya saa kumi (jana) tutampelekea Waziri taarifa ya ujenzi wa mradi huu kama alivyotuagiza. Kuhusu makandarasi mizigo tutachunguza ikiwa wapo basi hatua za kinidhamu zitachukuliwa,” alisema.

Injinia wa umwagiliaji wa Manispaa hiyo, Fransis Mugisha alisema, hawezi kueleza chochote kuhusu mradi huo licha ya kuwa ulijengwa kwa usimamizi wa ofisi yake.

“Sina ‘comment’ kwa sababu waziri ameagiza na kama kuna wahandisi mizigo basi sheria ipo,” alisema.

Juzi, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick kuwa ili mradi huo unahitaji Sh6 bilioni.     

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Bibi Jenista Mhagama (Mb), akimsikiliza mkazi wa Tegeta, Basihaya Jijini Dar es Salaam, Jumanne Malongo alipokuwa akimueleza jinsi wembamba wa mtaro huo unavyosababisha maji kujaa katika makazi yao, jana wakati alipofanya ziara kuangalia jinsi wilaya hiyo ilivyojiandaa kukabili maafa ya Mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda.

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Manisipaa kinondoni, Ando Mwakunga akimueleza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Bibi Jenista Mhagama (Mb), uharibifu wa “kalvati” katika eneo la Boko, Ununio Jijini Dar es Salaam, jana wakati Waziri huyo alipofanya ziara kuangalia jinsi wilaya hiyo ilivyojiandaa kukabili maafa ya Mvua zinazoendelea kunyesha jijini humo.

Mbowe Azungumzia Kasi ya Rais Magufuli.....Adai Kuwa Mpinzani Haimaanishi Upinge Kila Kitu


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amezungumzia kasi aliyoanza nayo rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli pamoja na baraza lake la mawaziri.

Akizungumza jana na mwandishi wa habari wa Azam TV, Mbowe alisema kuwa rais Magufuli ameanza vizuri kiutendaji na kwamba ameanza kuzifanyia kazi hoja zilizokuwa zikihubiriwa na Chadema ndani na nje ya Bunge.

“Hoja ya kubana matumizi ya serikali, hoja ya kupunguza sherehe za kitaifa, hoja ya kupunguza safari za nchi za nje kwa viongozi wetu, hoja ya kupunguza watumishi wa umma ambao hawana umuhimu, hoja ya kuwa na serikali ndogo. Haya mambo tulizungumza siku zote na hawa hawa wa Chama cha Mapinduzi ndio waliokuwa wanayapinga haya,” alisema Mbowe.

Mbowe alieleza kuwa dhana ya upinzani sio kupinga kila kitu kinachofanywa na serikali hivyo chama chake hakitakuwa tayari kupinga mambo mema yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano kama baadhi ya watu wanavyotarajia, bali kitajikita katika kujadili na kuibua hoja za msingi.

“Kuwa mpinzani sio kupinga kila jambo linalofanyika hata kama likiwa jema. Sasa sisi kama kambi rasmi ya upinzani bungeni na hata nje ya bunge ni wajibu wetu katika wakati wote ule kuhakikisha tunaisimamia serikali ili anachokisema rais kweli kitekelezwe kwa vitendo na isiwe hoja ya rais pekee,”alisema.

Hata hivyo, Mbowe alikosoa uteuzi wa baadhi ya mawaziri katika baraza la serikali ya awamu ya tano hususan Dk. Harison Mwakyembe ambaye wizara ya Uchukuzi aliyokua akiiongoza awali imekumbwa na sakata la upotevu wa makontena bandarini na Profesa Sospeter Muhongo ambaye amerudishwa katika wizara ya Nishati na Madini baada ya kujiuzulu katika nafasi hiyo wakati wa serikali ya awamu ya nne kufuatia sakata la Escrow.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Afanya Ziara ya Kushtukiza Hospitali ya Muhimbili Leo na Kukuta Mashine za CT Scan na MRI Zimeharibika Tena NA HIKI NDICHO KILITOKEA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee Ummy Mwalimu amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili leo na kukuta mashine za CT Scan na MRI hazifanyi kazi.

Katika ziara hiyo aliyoifanya asubuhi ya leo, alikutana na mzee wa miaka 90 ambaye alikuwa akisubiri huduma hiyo tangu jana.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Wa Hospitali hiyo, Lawrence Museru, mashine hizo ziliharibika tangu juzi na hivyo huduma zilisimama tangu jana asubuhi.

Tatizo kubwa katika machine ya CT Scan picha hazisomeki vizuri na MRI imeharibika spea ambazo kwa mujibu wa uongozi wa hospitali hiyo, matengenezo yanaanza leo.

Hata hivyo, Mwalimu ameagiza uongozi wa hospitali hiyo ya rufaa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa mashine hizi zinarudi katika hali yake ya kawaida.

Mashine hizo zimeendelea kuwa changamoto kwa hospitali hiyo licha ya Rais John Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza na kukuta hali kama ya leo.

Lowassa kuzunguka nchi nzima kuanzia kesho SABABU ZA MIZUNGUKO HIYO ZAELEZWA HAPA


Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa ataanza ziara ya kuzunguka nchi nzima kuwashukuru Watanzania kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 na kesho atakuwa Tanga.

Katika ziara hiyo, Lowassa ataambatana na viongozi waandamizi wa Chadema na Ukawa kuwashukuru wananchi kwa namna walivyounga mkono upinzani na ajenda nzima ya mabadiliko katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imesema kiongozi huyo atatoa shukrani zake kwa wananchi kwa jinsi wanavyoendelea kuweka matumaini yao kwa upinzani.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba wananchi bado wanaamini kwamba upinzani ndiyo nguzo imara wanayoitegemea katika kuwaletea mabadiliko ya kweli kwa ajili ya maendeleo yao na ustawi wa Taifa kwa ujumla.

“Wananchi wanastahili shukrani kwa imani hiyo kubwa ambayo ni ishara ya wazi kuwa matumaini yao kwa miaka mingine mitano yatasimamiwa na kuongozwa na upinzani imara kupitia Ukawa,” alisema Makene katika taarifa hiyo.

Alisema mbali na kupiga kura nyingi katika nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita, wananchi waliwachagua wabunge wengi wa upinzani wanaotokana na Ukawa. Alisema wabunge hao wameongeza nguvu kubwa ndani ya Bunge hususan kupitia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo itakuwa serikali mbadala.

Pia, alisema wananchi wameviamini vyama vya upinzani ili kusimamia na kuongoza halmashauri 34 nchi nzima, ikiwa moja ya misingi imara katika kupigania mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka.

Older Posts
© Copyright UDAKU WA DUNIA Published.. Blogger Templates
Back To Top