Jeshi la polisi Mkoa wa Kigoma linamshikilia mgombea wa udiwani kata ya Kibirizi kupitia ACT-Wazalendo kwa tuhuma za kumpiga mwanachama wa CCM, Sifa Iddi (25) na kumsababishia maumivu na kulazwa katika Hopitali ya Mkoa ya Maweni kwa matibabu.
Mgombea huyo anatuhumiwa kutenda kosa hilo Oktoba 11, mwaka huu eneo la Buronge Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinard Mtui, alisema wakati Sifa akiwa nyumbani kwao wakiendelea na shughuli zao mbalimbali, alifika mgombea wa udiwani wa ACT – Wazalendo, Rashid Ruhomvya na wenzake ya kuomba kura.
Kamanda Mtui alisema mlalamikaji alikataa kwamba wao hawawezi kumpa kura kwa sababu ni wanachama wa CCM badala yake watampa mgombea wa CCM.
Alisema baada ya majibu hayo, ilizuka tafrani ndipo mgombea huyo alipompiga Sifa mateke tumboni na kuanguka chini kisha akapoteza fahamu ambapo wasamaria wema walimchukua na kupeleka Kituo Kikuu cha Polisi na kupewa PF3 kwa ajili ya kupelekwa Hospitali ya Maweni.
Kamanda Mtui alisema hawawezi kimwachia mtuhumiwa kwa sababu mlalamikaji amelazwa hospitali na hali yake siyo nzuri.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo kata ya Kibirizi, John Edward, alisema Sifa hakupigwa na mgombea bali alikuwa anaumwa kwa muda mrefu.
Alidai kuwa hizo ni njama zilizopangwa kisiasa kutaka kumharibia mgombea wao.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment