Aliyekuwa kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Juma Mwapachu (pichani) , ametangaza rasmi kujiunga kambi ya muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) huku akifichua kuwa hivi sasa kuna mawaziri wengi wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, wanaukubali umoja huo.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe baada ya kukabidhi rasmi kadi katika lililokuwa tawi lake, Mikocheni jijini Dar es Salaam jana, Mwapachu alisema hivi sasa CCM imepoteza mwelekeo na ndiyo maana ameamua kuhama ili amuunge mkono mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa, kwa nia ya kuleta mabadiliko ya kweli.
Mwapachu alisema uamuzi kama huo unaweza kufanywa na mawaziri wengi baadaye ambao hivi sasa wanashindwa kufanya maamuzi magumu ili kutekeleza dhamira hiyo kwa sababu bado wako madarakani.
Hata hivyo, Mwapachu hakutaja majina ya mawaziri anaoamini kuwa wanaweza kuihama CCM.
Ukawa unaundwa na vyama vya NLD, NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ndicho kimemsimamisha Lowassa kugombea urais katika uchaguzi mkuu Oktoba 25. Mwapachu aliyewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM na pia kuwahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema sababu kubwa iliyomuondoa katika chama chake cha zamani ni udikteta ulioonyeshwa katika uteuzi wa wagombea urais kupitia chama hicho.
Alisema alisikitishwa kuenguliwa kimizengwe kwa Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal, pamoja na watu wengine kadhaa wenye sifa wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Mwapachu alisema halikuwa jambo la busara kwa CCM kuengua majina hayo na mengine kati ya 38 ya walioomba kuteuliwa kuwa wagombea urais wa chama hicho na kwamba, uamuzi huo wa kidikteta ulileta mpasuko wa kisiasa na kudhihirisha kuwa CCM ya sasa imeshapoteza mwelekeo na hilo lilianza kuonekana tangu mwaka 1995.
Alisema licha ya kuihama CCM, anaamini bado mchango wake utakumbukwa na kuahidi kushirikiana nacho katika shughuli za kimaendeleo ikiwa watamshikirisha.
Aliongeza kuwa CCM ni lazima itambue kuwa mabadiliko ni dhahiri Oktoba 25 na kwamba kuanzia sasa, yeye ataendelea kuwa muungaji mkono wa Ukawa chini ya Chadema.
Alisema kuhama kwa kada mwingine mkongwe CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru, ni mmoja wa watu wachache ambao hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliwaheshimu kutokana na fikra sahihi walizokuwa nazo kwa Chama na kwamba, kuhama kwake chama hicho ni ushahidi kuwa mambo hayaendi tena vizuri.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment