Rais wa shirikisho la mpira wa miguu duniani Joseph ‘Sepp’ Blatter kwa mara nyingine tena amewatolea maneno ya kuishambulia uingereza kwa kile anachosema ni chuki dhidi ya shirikisho hilo.
Akiongea na gazeti moja nchini Uswis, rais huyo wa FIFA ameponda chuki za waingereza dhidi ya shirikisho hilo huku akidai ilianza zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Blatter amesema mara baada ya waingereza kupitia kwa mgombea wao Sir Stanley Rous kupoteza kiti cha urais wa shirikisho hilo 1974 ndio kimekua chanzo cha chuki dhidi ya FIFA.
Blatter ambaye ametangaza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu huu kwa kashifa za rushwa zilizolichafua shirikisho na sura ya mpira duniani amekaririwa akisema hata skendo za ufisadi ziliibuliwa ili kumuweka kitimoto na kwamba asitulie.
Rais huyo mwenye miaka 79 hivi sasa amesema hawezi kujua kila kinachoendelea ndani ya shirikisho na kwamba binafsi sio fisadi.
Sio mara ya kwanza kwa Blatter kuwatupia maneno waingereza ambao hawakuridhika na ukweli kwamba walikosa nafasi ya uandaaji wa fainali za kombe la dunia 2018.
Chama cha soka nchini England, FA kimekuwa kikimpinga hadharani rais Blatter na sera zake kwa ujumla.
Source: shaffihdauda.co.tz
Post a Comment