Baada ya kamati ya sheria, maadili na hadhi za wachezaji ya shirikisho la soka Tanzania (TFF) chini ya mwenyekiti wake Richard Sinamtwa kutoa maamuzi wa kumtangaza mchezaji Ramadhani Singano ‘Messi’ kuwa yupo huru na anaweza kusajiliwa na klabu yoyote anayoitaka, uongozi wa iliyokuwa klabu yake (Simba) kupitia mwenyekiti wake wa usajili Zacharia Hans Poppe umetoa kauli juu ya uamuzi huo.
“Mimi binafsi nimelishughulia hili suala lakini nimesikitishwa sana na haya maamuzi na sikutegemea watu wa kwenye ile kamati hasa mwenyekiti kama wangefikia maamuzi kama yale. Kwasababu nilimchukulia mwenyekiti yule kama mtu mmoja mwenye kufuata haki, lakini leo sita sita kusema amekuwa ‘very bias’ na sijui amebadilika vipi kwasababu limezungumzwa na leo ilikuwa ni mara ya pili tu lakini tulishalizungumza huko nyuma na alilielewa vizuri”, amesema Poppe.
“Mambo yote tuliyoyazungumza kule nyuma anakuja kuyabadilisha leo kwasababu hataki kukubali kuwa tumemlipa pesa laki sita za mkataba wa nyumba ambao unataka tumlipe kwa miaka mitatu na bado mkataba haujaisha, sijui hata nisemeje, sikutegemea watu wa sampuli kama ile, kaliba kama ile wanaweza kutoa maamuzi kama yale”, ameeleza.
“Kipengele hakisemi tutampa nyumba, kipengele kinasema tutamlipa laki sita katika kipindi chake cha ‘contract’ ambacho ni miaka mitatu. Laki sita ya ‘accommodation’ kwa kipindi chote cha mkataba wake. Tulichotakiwa sisi ni kuthibitisha ni kwamba je, laki sita hiyo kapata? Lakini imeenda mbali zaidi hata kama hajapata mkataba wake bado haujaisha. Nafasi ya kulipa hiyo laki sita ipo na ‘hatuja-default’ chochote lakini cha ajabu ndio hicho”, alizidi kufafanua.
“Sisi hatuna cha kufanya maana kikao hicho kina ‘power’ na kikishafanya maamuzi hakuna namna ambayo unaweza kuyapinga wala namna ambayo unaweza kukatia rufaa katika vikao vyetu vya hapa. Neno lao ni la mwisho na watu wakitoa maamuzi ya vile basi inabidi yatekelezwe labda kama unataka kwenda CAF sasa hayo ni mambo ya kamati ya utendaji”, aliongeza.
“Mimi binafsi ningependa kulifatilia hili suala mpaka mwisho wake kwasababu nikitazama matukio ya huko nyuma maamuzi mbalimbali yamechukuliwa dhidi ya Simba halafu yanaishia hivi katikati halafu lawama zinakuja kwa Simba. Tukiangalia kwenye ule uamuzi wa Yondani ambapo tulipeleka mikataba miwili wakwetu na wale wengine walikuja na mkataba mwingine yalitoka maamuzi ya ajabu ya namna hiyohiyo sasa maamuzi ya namna hii yanatuumiza”, alimaliza.
Source: shaffihdauda.co.tz
Post a Comment