JUMUIYA ya Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) imesema wanasikitishwa na uteuzi wa baraza la mawaziri lililotajwa juzi na Rais John Magufuli na kudai kuwa, katika baraza hilo wamerudishwa wale mawaziri waliokumbwa na kashfa za ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.
Pia imesema katika baraza hilo hakuna uteuzi ambao umewiana hasa katika suala la usawa wa kijinsia na wala haukuzingataia Muungano uliokuwepo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Hamidu Bobali amesema wanashangaa kuwaona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Harson Mwakyembe kuwepo tena.
Amesema, Waziri Muhongo alikuwa anatuhumiwa na suala la Escrow na akajiuzulu halafu Magufuli amemrudisha tena kitu ambacho kinawakosesha amani.
“Inatusikitisha sana kitendo cha Rais wetu kumteua tena Waziri Muhongo kurudi tena wizarani hapo wakati alikuwa na kashfa kubwa ya escrow lakini amerudishwa tena inaonyesha Magufuli pia pamoja na kusifiwa juu ya utendaji wake hayuko makini,”amesema Bobali.
“Pamoja na Muhongo pia Waziri Mwakyembe alikuwa katika wizara ambayo sasa hivi inakubwa na matatizo makubwa ya kupitisha makontena na wakati alikuwa waziri katika wizara hiyo, hilo lilitosha kwa Magufuli kufanya upembuzi wa Mawaziri. Hao wote hawakufaa tena kuridi kuwa mawaziri,” amesema.
Ameongeza kuwa, wanasikitishwa sana kwani ile kasi ambayo Magufuli alianza nayo wanaiona inakufa siku si nyingi kwa kuwarudia tena mawaziri hao mizigo.
“Wananchi tunasikitika sana kwa kuwa tulimuamini Rais Magufuli lakini imani hiyo inakaribia kukatika kutokana na kurudishwa kwa mawaziri hawa na kusababisha kasi kupungua,”ameeleza
Aidha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo hakuwahi kupatikana na hiyo ya Escrow kwani alijiuzulu mwenyewe. Kwa kuhofia kupatikana na hatia.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti huyo alizungumzia mgogoro uliokuwepo Zanzibar na kusema kuwa Baraza la vijana wa chama hicho kwa kushirikiana na vyama vinavyunda Umoja wa Katiba Wananchi (Ukawa) wameandaa mkutano juu ya kuzungumzia mgogoro huo.
“Tunafurahishwa na mazungumzo yanayoendelea kati ya viongozi kwetu wa huko Zanzibar lakini baraza letu limeandaa mkutano huo ili kuzungumzia suala hili,”amesema Bobali
Hata hivyo Bobali amesema wanamuomba Rais Magufuli kuliingilia kati suala la Zanzibar kwani kutokufikia kikomo kunasababisha mambo mengi kurudi nyuma ikiwa moja na uchumi kushuka.
“Jumuiya ya vijana inawatahadharisha wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuacha mara moja kauli chafi na vitendo vya kichochezi vinavyofanywa na wanachama hao kwani vinaweza kuamsha hasira za vijana wa CUF Zanzibar,” amesema Bobali.
Post a Comment