Uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kueleza kwa kina namna safari holela za nje ya nchi zinavyoligharimu taifa mabilioni ya fedha, umeianika wazi Serikali iliyopita ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini.
Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya kiasiasa wanasema kuwa ujasiri wa Rais Magufuli kueleza bila kificho jinsi safari za nje zinavyogharimu taifa kabla ya kutangaza msimamo mkali wa kuzidhibiti umedhihirisha pasi na shaka kuwa rais huyo mpya amedhamiria kubana matumizi holela ya fedha za serikali na badala yake kuzielekeza katika shughuli za maendeleo kwa nia ya kuboresha maisha ya Watanzania.
Wakati akilihutubia Bunge la 11 Ijumaa iliyopita kisha kulizindua rasmi, Rais Magufuli aliwataka wabunge na Watanzania wote wamuunge mkono katika uamuzi wake wa kupiga marufuku safari holela za nje huku akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo, fedha nyingi zinazopotea zinaweza kutumiwa katika kuboresha huduma za jamii.
Akitaja kwa mifano jinsi safari hizo za vigogo nje ya nchi zinavyoligharimu taifa, Magufuli alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015 peke yake, taifa lilitumia Sh. bilioni 356.324 kugharimia safari hizo; kiasi ambacho kwa maelezo yake, kingetosha kujenga barabara ya lami ya urefu wa kilomita 400 na pia kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya maji, elimu na afya.
Alisema mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo ulikuwa ni tiketi za ndege (Air ticket) Sh. bilioni 183.160, mafunzo nje ya nchi Sh. bilioni 68.612 na posho za kujikimu (Per Diem Foreign) Sh. bilioni 104.552.
Magufuli alizitaja wizara na taasisi za umma zilizoongoza kwa kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari za nje ya nchi kuwa ni Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, sasa safari hizo ni marufuku na pale inapolazimu, ni lazima kibali kitoke kwake au kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, na kwamba, kuanzia sasa watakaokuwa wakijumuishwa kwenye misafara ya lazima nje ya nchi ni watu muhimu tu wanaohitajika katika safari husika.
“Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu na umeme. Mfano, fedha hizi zingetosha kutengeneza kilomita 400 za barabara za lami. Tujiulize, zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? nyumba za walimu ngapi? Madawati mangapi?” alihoji Rais Magufuli wakati akielezea suala hilo bungeni na kuongeza:
“Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.”
Alivyo "Ivua Nguo" Serikali ya Awamu ya nne
Hotuba ya Rais Magufuli aliyoitoa mwishoni mwa wiki inaonyesha wazi kuwa misafara ya mara kwa mara ya viongozi mbalimbali kwenda nje ya nchi ilikuwa ikiligharimu taifa kwa kiasi kikubwa kwani fedha hizo zingefanya mambo mengi kwa manufaa ya nchi badala ya kunufaisha vigogo wachache.
Wakati fedha nyingi zikitumika kwa safari hizo, bado hali ni mbaya katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii; mambo ambayo Magufuli amesisitiza kuwa kamwe hatakubali kuyaruhusu katika serikali yake ya awamu ya tano.
Fedha hizi zilizotafunwa na viongozi mbalimbali kupitia safari za nje (Sh. bilioni 356) zingeweza kufanikisha mambo mengi ya maendeleo kwa taifa kama ifuatavyo.
1. Madawati 3,098,469
Bei ya dawati moja linalochukua wanafunzi watatu wa shule za msingi huwa ni kati ya Sh. 80,000 hadi 150,000, wastani wake ukiwa ni Sh. 115,000.
Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha zilizotumika kwa safari za vigogo (Sh. bilioni 356) zingetumika kununua madawati, maana yake yangepatikana madawati 3,098,469 na hivyo kumaliza tatizo hilo katika shule za msingi nchini.
2. Visima vya maji safi 35,632
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, gharama za kuchimba kisima cha maji safi huwa ni kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000 kwa kina cha mita moja, kutegemeana na jiografia ya eneo husika.
Kwa sababu hiyo, kama kisima kitakuwa na urefu wa mita 100 na kitachimbwa kwa Sh. 100,000 kwa kila mita moja, maana yake kiasi cha fedha kitakachohitajika ni Sh. milioni 10.
Hivyo, ikiwa fedha za safari za nje (Sh. bilioni 356) zingetumika kuchimba visima vya maji safi vya thamani hiyo, maana yake vingepatikana visima 35,632. Visima hivyo vingegawanywa sawa katika wilaya 133 nchini, maana yake kila wilaya ingepata mgawo wa visima 268.
3.Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh. 4,219,500 kwa mwaka. Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni Sh. 2,099,500 kwa ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh. 620,000 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.
Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za safari za nje alizozitaja Rais Magufuli zingetumika kuwapa mikopo wanafunzi wa elimu ya juu kama wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini wanaolipwa asilimia 100, maana yake wanufaika kwa mwaka wangekuwa wanafunzi 84,447.
4.Magari ya kubebea wagonjwa
Mwaka jana, Agosti 28, kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya takriban Sh. milion 76.
Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha zilizotajwa na Rais Magufuli kuwa zilitumika kusafirisha vigogo nje ya nchi zingeelekezwa katika kununua magari ya wagonjwa kama walilopata msaada Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, maana yake taifa lingepata magari mapya ya wagonjwa 4,688.
5.Zahanati 4,454.
Septemba 16 mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba, alisema kuwa katika jimbo lake, wamekamilisha ujenzi wa zahanati za vijiji kadhaa kwa wastani wa Sh. milioni 80 kwa kila moja.
Kwa sababu hiyo, kama fedha za safari alizozitaja Rais Magufuli kuwa zilitumika kusafirisha vigogo nje ya nchi (Sh. bilioni 356) zingetumika kujengea zahanati kama za jimbo la Bumbuli, maana yake taifa lingepata zahanati mpya takriban 4,454.
6.Maabara shule za Sekondari 6,122
Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, aliwahi kukaririwa Aprili 20, 2015, akisema kuwa shuleni kwake walikamilisha ujenzi wa maabara mojawapo kwa Sh. milioni 58.2.
Kwa sababu hiyo, kama fedha za safari kusafirisha vigogo nje ya nchi wakati wa Rais Kikwete mwaka juzi na mwaka jana zilizotajwa na Magufuli (Sh. bilioni 356) zingetumika kujenga maabara za shule za sekondari kama Sekondari ya Tandika, maana yake zingejengwa maabara 6,122 na kumaliza tatizo hilo nchini.
7.Mikopo kwa wajasiriamali( Kila mmoja 500,000)
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali wanawake ni ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Hata hivyo, kama ingetokea serikali ya Rais Kikwete ingesitisha matumizi ya fedha za safari za nje kwa viongozi alizozitaja Rais Magufuli (Sh. bilioni 356) na badala yake kuzielekeza katika kuwakopesha mitaji wajasiriamali wanawake kwa kiasi cha Sh. 500,000 kila mmoja, maana yake wanufaika wangekuwa ni kina mama 712,648.
8.Bodaboda aina ya Boxer
Bei ya juu ya pikipiki aina ya Boxer zinazotumika kwa biashara ya bodaboda ni Sh. milioni 2.5.
Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za posho za safari alizozitaja Magufuli kuwa zilitumika katika miaka ya fedha ya 2013/2014 na 2014/2015 (Sh. bilioni 356) kwa ajili ya safari za vigogo nje ya nchi zingeelekezwa katika kununulia pikipiki hizi kwa ajili ya kuwakopesha vijana wanaotoa huduma ya usafiri wa bodaboda, maana yake zingepatikana pikipiki za aina hiyo takriban 142,530.
9.Vipimo CT-Scan 356
Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa mashine za kipimo maarufu cha CT-Scan, aina ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi bilioni moja.
Hivyo, kama Sh. bilioni 356.324 alizozitaja Rais Magufuli kuwa zilisafirisha vigogo nje ya nchi zingeelekezwa kununua vipimo hivyo, maana yake zingepatikana CT-Scan 356 za thamani ya Sh. bilioni moja kila moja na kufungwa katika hospitali zote za rufaa nchini na nyingine nyingi zikaelekezwa katika hospitali za wilaya na pia vituo vya afya.
10.Daladala Toyota Coaster 6,089.
Kwa mujibu wa mtandao wa Trade Car View, bei ya kununua gari aina ya Toyota Coaster iliyotumika lakini iliyo katika hali nzuri ni dola za Marekani 27,896, sawa na takriban Sh. 58,513,255.
Kama fedha zilizosafirisha vigogo nje ya nchi katika miaka ya fedha ya mwisho ya Rais Kikwete (Sh. bilioni 356) zingetumika kununulia gari hizi kwa ajili ya kuwapatia wajasirimali wanaotoa huduma ya usafiri wa daladala nchini, maana yake zingepatikana daladala 6,089.
==> Chanzo: Nipashe
KUJIUNGA NA KINYANG'ANYIRO CHA PIKIPIKI AINA YA BOXER BONYEZA PICHA CHINI YA MANENO HAYA NA UIBUKE MSHINDI,BONYEZA MARA NYINGI UWEZAVYO KUIBUKA MSHINDI;
Post a Comment