KWA VYOMBO VYA HABARI
Tumepokea taarifa kwamba Balozi Seif Ali Iddi amehojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio France International (RFI) na kusema kwamba eti viongozi wa CCM na CUF WAMEKUBALIANA UCHAGUZI ZANZIBAR URUDIWE, na kinachojadiliwa hivi sasa ni NANI ASIMAMIE UCHAGUZI WA MAREJEO kwa sababu ZEC ya JECHA INAONEKANA KUTOAMINIKA.
Tunapenda kuwawekea wazi Wazanzibari wote kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote, ni za uzushi na wazipuuze.
Msimamo wa CUF na Maalim Seif Sharif Hamad uko pale pale kwamba HAKUNA KURUDIWA UCHAGUZI na kwamba MSHINDI HALALI WA UCHAGUZI WA TAREHE 25 OKTOBA, 2015 ATANGAZWE NA KUAPISHWA.
Kauli za Balozi Seif Ali Iddi ni za kutapatapa zianzolenga kuwatuliza wana-CCM ambao wanaonekana kukata tamaa baada ya kushindwa vibaya na CUF kwenye uchaguzi mkuu wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Madiwani uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kwenye uchaguzi mkuu wa Urais wa Zanzibar, mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alimbwaga vibaya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa zaidi ya kura 25,000.
Balozi Seif Ali Iddi mwenyewe akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM anatuhumiwa na wana-CCM kushindwa kazi na kukisababishia chama chao kushindwa vibaya kuliko wakati wowote katika historia ya chaguzi za Zanzibar.
Lakini kama hilo halitoshi, wana-CCM wanamtuhumu Balozi Seif na wajumbe wengine wa Kamati ya Kampeni aliyokuwa akiiongoza kusimamia matumizi mabaya ya kiasi kikubwa cha fedha za kampeni za Chama hicho ambazo sehemu kubwa walimdanganya mgombea wao, Dk. Ali Mohamed Shein, kwamba zimetumika kuleta ushindi wa CCM kisiwani Pemba lakini kumbe ziliishia katika mifuko ya watu binafsi.
Haistaajabishi kwamba sasa Balozi Seif Ali Iddi ameamua kuja na njia ya kutoa taarifa za udanganyifu ili kujinusuru na mzigo wa tuhuma za kushindwa kazi na kusimamia matumizi mabaya ya fedha za kampeni kutoka kwa CCM wenzake.
CUF tunamtaka Balozi Seif Ali Iddi awache kudanganya umma na badala yake awajibu CCM wenzake kwa nini amekitia chama hicho aibu na fedheha kubwa ya kupata kipigo kibaya katika uchaguzi kilichopelekea CCM kupoteza majimbo tisa (9) kisiwani Unguja na Dk. Ali Mohamed Shein kushindwa uchaguzi wa Urais wa Zanzibar kwa zaidi ya kura 25,000 huku wakidai kutumia mamilioni ya fedha ambazo hawana maelezo zimetumika vipi.
CUF tunawataka Wazanzibari kutobabaishwa na kauli za kushindwa kazi za Balozi Seif Ali Iddi na watulie wakijua kuwa ufumbuzi wa haki wa uchaguzi mkuu utapatikana kwa kutangaza matokeo ya kura kwa majimbo yaliyobakia na hatimaye mshindi kutangazwa na kuapishwa.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
MKURUGENZI WA MAWASILIANO - CUF
26 NOVEMBA, 2015
KUJIUNGA NA KINYANG'ANYIRO CHA PIKIPIKI AINA YA BOXER BONYEZA PICHA CHINI YA MANENO HAYA NA UIBUKE MSHINDI,BONYEZA MARA NYINGI UWEZAVYO KUIBUKA MSHINDI;
Post a Comment