Mwenyekiti wa Chadema, mh Freeman Mbowe amemtaka Rais Kikwete kutovuruga amani ya nchi na badala yake amemtaka aondoke madarakani na kuiacha nchi ikiwa salama.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana jioni katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbogwe, wilayani Geita.
Alisema Rais Kikwete anatakiwa aondoke madarakani salama kama walivyofanya marais wenzake wastaafu.
“Rais Kikwete ameamua kuwa mpiga debe wa Magufuli (mgombea wa CCM), sasa mimi naomba nimjibu yeyekama mpiga debe na si rais,” alisema Mbowe.
Alisema Rais Kikwete ameamua kuwaaminisha Watanzania kuwa wapiga kura wapo milioni 28 badala ya milioni 22 kama ilivyotangazwa na Tume ya Taifa ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
“Sasa nataka kumuuliza Rais Kikwete hao wapiga kura wengine milioni sita wametoka wapi?” alihoji Mbowe na kuongeza:
“Naomba kumwambia Rais Kikwete kuwa hii nchi si yake, hii nchi si ya CCM na hii nchi si ya familia yake...hii ni nchi ya Watanzania,” alisema.
Alisema hatua ya Rais Kikwete na CCM inayoungwa mkono na Nec kuwataka wananchi wapige kura na kuondoka vituoni haiwatendei haki Watanzania.
“Kikatiba Watanzania wana haki ya kulinda kura zao kwa sababu zile ni kura zao, nashangaa Rais Kikwete anawaambia watu waondoke,” alisema.
Mbowe, aliwaomba Watanzania wote kwenda kwenye vituo kwa ajili ya kupiga kura ikiwa ni pamoja na kuzilinda kura zao.
Pia alisema anashangazwa na kauli ya Rais Kikwete ya kuliagiza Jeshi la Polisi kuwaondoa wananchi kwa nguvu katika vituo vya kupigia kura.
“Hao askari walioagizwa na Rais Kikwete, nao wana watoto na familia zao, naomba nikwambie Rais Kikwete kuwa huwezi kuzuia mabadiliko. Zimebaki siku 11, Mungu atajibu maombi yetu...nawaambia wananchi nendeni mkapige kura kaeni mita 200 lindeni kura zetu,” alisema.
Akiwa mjini Dodoma jana wakati wa kilele cha Mwenge wa Uhuru kilichoenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais Kikwete alitaja idadi kubwa ya wapiga kura kuliko iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Hata hivyo, jana jioni Ikulu ililitolea ufafanuzi suala hilo na kudai kuwa idadi kamili ya wapiga kura ni milioni 22 na si vinginevyo.
"..... Katika Kilele cha mbio za mwenge wa uhuru , kumbukumbu ya Baba wa Taifa , Mwalimu JULIUS Nyerere na wiki ya vijana Kitaifa, Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake amezungumzia idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura.
"Kwa uhakika amesema kuwa idadi ya wapiga kura ni 22,751, 292 kwa upande wa Bara na 503,193 waZanzibar . Hii ndiyo idadi kamili ambayo imo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais na hii ndiyo idadi kamili kama ilivyotolewa na Tume ya Uchaguzi Tanzania .." Ilisema Sehemu ya Tamko hilo la Ikulu jana.
KUJIUNGA NA KINYANG'ANYIRO CHA PIKIPIKI AINA YA BOXER BONYEZA PICHA CHINI YA MANENO HAYA NA UIBUKE MSHINDI,BONYEZA MARA NYINGI UWEZAVYO KUIBUKA MSHINDI;
Post a Comment