Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, ametinga katika Jimbo la Monduli, mkoani Arusha ambalo ni ngome kuu ya mgombea urais aliyesimamishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chadema, Edward Lowassa.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika jana katika eneo la Mto wa Mbu, wilayani Monduli, Dk. Magufuli alisema ataibuka na ushindi wa kishindo uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kuapishwa kuwa rais wa awamu ya tano wa Tanzania.
“Hadi sasa nimeshapata uhakika wa kushinda kwa asilimia 85 na kinachofuata ni kuongeza ushindi huo hadi kufikia asilimia 99. Wananchi wa Monduli msihangaike kumpigia kura mgombea urais ambaye atashindwa na badala yake mnichague mimi kwani nina uhakika wa kushinda kwa kishindo. Hapa kwangu ni kazi tu” alisema.
Dk. Magufuli aliwashukuru wananchi wa Mto wa Mbu kwa kumpa mapokezi mazuri licha ya mkutano huo kufanyika asubuhi wakiwa katika harakati za uzalishaji.
ARUSHA MAKOMBORA CCM
Katika hatua nyingine, mgombea huyo wa urais wa CCM aliwarushia mashambulizi baadhi ya viongozi ndani ya CCM kwamba wameshindwa kutatua matatizo ya wananchi hivyo kusababisha waichukie serikali.
Alisema ingawa Jimbo la Monduli linaheshimika sana kutokana na kazi kubwa zilizofanywa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Hayati Edward Moringe Sokoine, lakini tangu afariki huduma nyingi zimedorora.
“Leo hii mmefikia hatua wananchi wa Monduli wanafunzi wanarudishwa nyumbani kwa michango ya maharage na unga hii ni aibu sana kwa kweli….jimbo hili linahitaji ukombozi na nawaambia wananchi wa jimbo hili msinye makosa amleteni Namelock Sokoine (mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM,” alisema.
ATEMBELEA KABURI LA SOKOINE
Kabla ya kuhutumia mkutano mkubwa wa Monduli Mjini, Dk. Magufuli alikwenda kutembelea kaburi la Sokoine nyumbani kwake Monduli Juu na kisha kuzungumza na familia yake.
Aliosema Sokoine alichukia rushwa na ufisadi na aliwatumikia watanzia kwa moyo wake wote.
APATA MAPOKEZI MAKUBWA ARUSHA
Dk. Magufuli alipata mapokezi makubwa katika mji wa Arusha ambao unaelezwa kuwa ngome kuu ya Chadema mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Edward Lowassa.
Dk. Magufuli aliwasili katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa jana saa 9:00 alasiri na kukuta idadi kubwa ya wananchi wakimsubiri, tofauti na matarajio ya watu wengi kwamba huenda angekosa watu uwanja hapo kiasi cha kusababisha msongaamano mkubwa ndani na nje ya uwanja.
Umati huo ulimshangaza hata Dk. Magufuli mwenyewe ambaye alisema ni amapokezi yaliyovunja rekodi.
Dk. Magufuli alisema kuna watu walikuwa wakiwatisha watu kwamba mkutano huo ungekosa mahudhurio mazuri lakini mambo yamekuwa kinyume na matarajio yao.
Mgombea huyo wa urais wa CCM alipata mapokezi makubwa tangu alipoingia mkoani hapa Jumatatu jioni na kuanza kuhutubia katika Jimbo la Karatu ambalo pia ni ngome ya Chadema.
Mgombea huyo jana pia alifanya mikutano katika majimbo ya Monduli, Longido na Arusha Mjini, ambako kote alipata mwitikio mkubwa wa wananchi.
“Nimetembea maeneo mbalimbali hapa Arusha nilianzia Karatu wamefunika, Monduli wamefunika, Longido wamefunika na nyinyi hapa Arusha Mjini mmefunika nawashukuru kwa mapokezi haya ya aina yake wananchi wa Arusha naondoka na deni,” alisema Dk. Magufuli wakati akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana.
Mgombea huyo aaliwaambia wakazi wa Arusha kwamba wazee wa Kimasai wamemwombea baraka zote awe Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anaamini atashinda kwa kishindo.
“Nafahamu mji wa Arusha mnahitaji mabadiliko ya maisha bora kwa wote ambayo mtu pekee anayeweza kuyaleta ni mimi. Nitaubadili mji huu kuwa mfano kwa nchi za Afrika Mashariki na serikali yangu itahakikisha inatandaza barabara za lami ili kuufanya uwe wa kitalii kwelikweli,” alisema.
SOURCE: NIPASHE
:
Post a Comment