George Aloyce Kimaryo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kusambaza taarifa zauongo kupitia katika kundi la Adios la mtandao wa WhatsApp kuwa Mwanafunzi wa Chuo cha DIT, Benedict Angello Ngonyani amejitokeza kwa mara ya pili mahakamani na kuishangaza kwa kumtaka Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange ajitokeze na kukanusha kuwa amelishwa sumu.
Wakili wa Serikali Jacquline Nyantori akishirikiana na Wakili Mwandamizi wa TCRA, Johannes Kalungula walidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa Oktoba 13,2015 katika mtandao huo wa kijamii mshtakiwa huyo alisambaza taarifa hiyo kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya Mtandao namba 14 ya 2015.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 3, 2015 kwa ajili ya kutajwa na kufikiria juu ya maombi ya dhamana.
Mwanafunzi huyo wa Chuo cha DIT, Benedict Angello Ngonyani yeye anakabiliwa na kesi ya kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa WhatsApp na Facebook kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange amelishwa sumu.
Tangu afikishwe mahakamani hapo kwa mara ya kwanza siku 14 zilizopita leo yaani jana ndiyo alipanda kwa mara ya pili kizimbani mbele ya Hakimu Respicius Mwijage ambapo Wakili Nyantori alidai kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake bado haujakamilika.
Nyantori alidai katika kesi hiyo, kuwa kesi hiyo inahusisha mtandao bado wanakusanya taarifa ambazo ni za muhimu kupitia mfumo huo.
Hata hivyo wakili wa kujitegemea, Mnyela Abdallah alijitokeza mahakamani hapo na kujitambulisha kuwa yeye atakuwa wakili wa mshtakiwa huyo atakayemtetea kwenye kesi hiyo na akajulishwa kuwa mteja wake amewekewa zuio la dhamana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu Mwijage aliuambia upande wa mashtaka kuwa uliweka zuio hilo la dhamana na kutoa sababu ndani ya siku hizo 14 na kuwaambia kuwa sasa kuna umuhimu wa kulijadili dhamana ya mshtakiwa huyo na kitu ambacho kinapelekea andelee kuzuiwa kwa dhamana yake maana lazima kuwepo na sababu hivyo aliwataka Novemba 3,2015 kesi itakapotajwa kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la, waeleze sababu.
Ngonyani amekuwa ni mshitakiwa wa kwanza kufikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka kupitia sheria hiyo mpya ya mtandao ambayo inazuia mtu yoyote kusambaza ama kuchapisha data, taarifa za uongo, uzushi na zile ambazo hazijathibitishwa ama hazina chanzo pamoja na picha za matusi katika mitandao ya kijamii.
Katika kesi hiyo, Ngonyani anadaiwa kuwa Septemba 25,2015, jijini Dar es Salaam, alisambaza taarifa za uongo kupitia mitandao ya WhatsApp na Facebook kuwa Jenerali Mwamunyange amelishwa sumu na kwamba amepelekwa Nairobi Kenya kwa matibabu wakati akijua taarifa hizo zilikuwa na lengo la kupotosha umma.
Mbali na kesi hiyo, Mshtakiwa Raia wa China, Royce Lee na raia wa Pakistani Iqbal Wasif na Mohamed Jamil wamepandishwa kizimbani mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi tofauti za kuingiza mitambo ya kielektroniki ya mawasiliano nchini bila ya kuwa na leseni kutoka TCRA, wakaisimika na kutoa huduma za simu za Kimataifa kinyume cha sheria na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh 500 milioni.
KUJIUNGA NA KINYANG'ANYIRO CHA PIKIPIKI AINA YA BOXER BONYEZA PICHA CHINI YA MANENO HAYA NA UIBUKE MSHINDI,BONYEZA MARA NYINGI UWEZAVYO KUIBUKA MSHINDI;
Post a Comment