Katika hali isiyo ya kawaida, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, amemmwagia sifa Mbunge wa Jimbo hilo, Augustine Mrema kwamba ni kiongozi mchapakazi mwenye rekodi nzuri ambaye alisimamia haki wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Mgombea huyo aliwaambia wakazi wa Vunjo, mkoani Kilimanjaro jana kuwa kama wakishindwa kabisa kumchagua mgombea wa CCM, Innocent Shirima, ni heri wampe kura zao Mrema kwani ana moyo mwema na amewafanyia mengi wananchi wa jimbo hilo.
Mrema anawania ubunge wa jimbo hilo kupitia Tanzania Labour Party (TLP).
Akizungumza na wakazi hao maeneo ya Himo, Dk. Magufuli alisema Mrema amekuwa mtetezi mkubwa wa wananchi wa jimbo hilo anapokuwa bungeni, tofauti na mgombea ubunge kupitia NCCR-Mageuzi anayeungwa mkono na Ukawa, James Mbatia.
“Mimi nampenda sana Mrema hata kama yuko chama kingine, maana ni mpambanaji, ana shukrani sana na ni msema kweli, mkiona shida kabisa kumchagua Shirima, basi bora mumpe Mrema na mimi huyu Innocent nitampa kazi nyingine,” alisema na kuongeza:
“Mimi nitakuwa rais mvua inyeshe isinyeshe, kwa hiyo endapo mtamchagua mgombea wa CCM, Shirima mimi siwezi kumwacha Mrema hivi hivi, nitamteua, maana rais ana nafasi nyingi sana za uteuzi….. namheshimu sana Mrema na dhamira yangu itanisuta sana kama atashindwa ubunge na nisimteue.”
“Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, Shirima ndiye anawafaa hapa Vunjo, lakini mkishindwa kabisa kumchagua basi mpeni Mrema, maana amewasaidia sana,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli asimamisha msafara kumsalimia Mrema wakati msafara wake (Magufuli) ukitokea Himo Vunjo kuelekea Mwanga kwenye mkutano mwingine.
Mrema wakati huo alikuwa amekaa njiani na wafanyabiashara wadogo wadogo jirani kabisa na mizani ya Himo ndipo msafara wa Magufuli ulimfuata eneo hilo.
Dk. Magufuli alimfuata Mrema na kumpa nafasi ya kuzungumza, ndipo alipowaambiwa wananchi hao kwammba wasifanye makosa kwani rais anayefaa ni Dk. John Magufuli.
Mrema alisema ujio wa mgombea huyo jimboni humo ni neema kwani Dk. Magufuli amekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Vunjo kwa kuwatengenezea barabara za lami.
Mrema aliorodhesha kilomita za lami za jimbo hilo ambazo zimejengwa kwa usimamizi wa Dk. Magufuli, hali iliyoibua shangwe na nderemo kutoka kwa wafanyabiashara wa eneo hilo wengi wao wakiwa wanawake.
Chama chake cha TLP kimesimamisha mgombea urais ambaye ni Maxmilian Lyimo.
Hii si mara ya kwanza kwa Mrema kumpigia debe mgombea urais wa CCM wakati chama chake kikiwa kimesimamisha mgombea.
Mwaka 2010 Mrema alikuwa akimpigia debe Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa akiwania muhula wa pili wa urais unaomalizika mwezi huu, ingawa chama chake kilimsimamisha mgombea urais, Mutamwega Mgahywa.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment