Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Ligi kuu Tanzania bara imeanza kunoga, baada ya kumalizika kwa michezo ya mzunguko wa nne wikendi iliyopita, Jumatano hii ligi hiyo inaendelea kwa michezo 7 kuchezwa katika miji tofauti. Ni timu 3 tu ambazo hazijaangusha pointi hadi sasa.
Vinara Yanga SC wamekusanya alama 12 sawa na timu za Azam FC na Mtibwa Sugar, timu hizo zimeshinda gemu zao zote nne zilizopita na kwanza msimu kwa 100% ya ushindi. African Sport ya Tanga imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza msimu huu baada ya kuishinda Ndanda FC goli 1-0 Jumapili na kuziacha Coastal Union na JKT Ruvu katika kundi la timu ambazo bado hazijaonja ‘ladha’ ya ushindi msimu huu.
Mgambo imekusanya alama nne baada ya kufanikiwa kupata sare katika gemu moja na kushinda moja, imeshindwa katika michezo mingine miwili sawa na Mbeya City na Ndanda FC.
MTIBWA SUGAR v YANGA SC
Ni moja ya mechi kali katika raundi ya tano msimu huu. Mechi hii itazikutanisha timu zenye uwiano sawa wa pointi katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro Jumatano ya leo. Yanga ina wastani wa magoli 10 ya kufunga na kufungwa kwa maana wamefunga magoli 11 na kuruhusu nyavu zao mara moja.
Mtibwa ipo katika nafasi ya tatu ikiwa na wastani wa magoli manne ya kufunga na kufungwa. Kikosi cha kocha, Mecky Mexime kimefanikiwa kufunga jumla ya magoli 6 na kuruhusu mawili katika gemu nne zilizopita. Huo utakuwa mchezo wa tatu mfululizo kwa Mtibwa kucheza katika uwanja wa nyumbani wakati Yanga watakuwa nje ya uwanja wa Taifa kwa mara ya kwanza msimu huu.
“Yanga ni timu nzuri ila hawatishi, tutaendelea kuwafunga kila wanapokuja Morogoro” ni maneno ya msemaji wa Mtibwa, Thobias Kifaru ambaye timu yake haijapoteza mchezo dhidi ya Yanga tangu mwaka 2009 katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Yanga upande wao wamekuwa na ndoto ya kushinda gemu 10 mfululizo.
SIMBA SC vs STAND UNITED
Ni mechi nyingine kali ambayo itapigwa leo katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba imepeleka malalamiko yake kwa Shirikisho la soka nchini, TFF ikiwalalamikia waamuzi waliochezesha pambano lao la Jumamosi iliyopita dhidi ya mahasimu wao Yanga.
Katika mchezo huo, Simba ilipoteza kwa kulazwa 2-0 na hivyo kuporomoka katika msimamo kutoka nafasi ya pili hadi ya nne wakiwa na alama 9 baada ya kucheza gemu nne. Wataikabili Stand United ambayo imeshinda michezo miwili mfululizo na kuruka hadi katika nafasi ya sita wakiwa na alama 6.
Amri Kiemba, Nassoro Chollo, Haroun Chanongo, Elius Maguli wataungana na kocha wao, Mfaransa, Patrick Liewig kuikabili timu yao ya zamani. Simba haijawahi kuifunga Stand katika michezo miwili waliyokutana katika ligi ya msimu uliopita.
Walilazimishwa sare ya 1-1 katika uwanja wa Taifa na kuchapwa 1-0 katika uwanja wa Kambarage, Shinyanga katika mchezo wa marejeano. Stand imefunga magoli matatu tu msimu huu (yote yamefungwa na Maguli) na wameruhusu magoli matatu katika nyavu zao.
Upande wa Simba, kiufungaji hawajatofautiana sana na Stand kwani licha ya kufunga magoli 6 ni wachezaji wawili tu waliofanikiwa kufunga magoli hayo, Mganda Hamis Kiiza ambaye pia anashikilia kilele cha orodha ya wafungaji msimu huu amefunga magoli matano na kiungo/mlinzi, Justice Majabvi amefunga goli moja. Simba imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.
AZAM FC v COASTAL UNION
Coastal wanasafa kupata ushindi wa kwanza msimu huu. Wakiwa chini ya kocha, Mganda, Jackson Mayanja timu hiyo ya Tanga ilipoteza michezo miwili ya ugenini na wakaambulia sare mbili katika michezo miwili waliyocheza uwanja wao wa nyumbani, Mkwakwani.
Coastal Union wanakutana na Azam ambao wameshinda gemu zote nne zilizopita. Azam iliifunga Coastal 4-0 katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi msimu wa 2013/14, wakashinda tena 2-0 msimu uliopita. Coastal haijafunga goli lolote msimu huu na wameruhusu nyavu zao mara 3. Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 12 sawa na timu za Yanga na Mtibwa hadi sasa imefanikiwa kufunga juma ya magoli 7 na kuruhusu mawili katika nyavu zao.
Azam inaweza kwenda kileleni mwa msimamo wa ligi endapo itashinda mechi yao ya leo halafu Mtibwa na Yanga zikatoka sare kwenye mchezo wao kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro kwani endapo mtibwa na Yanga zikitoka sare zitakuwa na pointi 13 na Azam kama watashinda leo watafikisha pointi 15.
Mambo si mazuri kwa kocha wa Coastal Union, Jackson Mayanja kwani timu yake haina uwezo wa kufunga magoli, anaweza kutimuliwa kama mambo yatazidi kwenda ‘mrama’.
AFRICAN SPORT v JKT MGAMBO
Tanzania Prisons iliichapa 1-0 Mbeya City FC katika mchezo wa kwanza wa ‘mahasimu wa mji’ msimu huu, kisha Simba ikakubali kipigo cha 2-0 kutoka kwa Yanga, ‘Derby’ ya tatu itapigwa leo Jumatano katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati kikosi cha Sanifu Lazaro kitakapo wakabili maafande wa JKT Mgambo wanaonolewa na Bakari Shime.
Sport imepata ushindi wa kwanza msimu huu siku ya Jumapili baada ya kupoteza michezo mitatu mfululizo ya kwanza. Ikiwa imeruhusu magoli matano na kufunga goli moja tu, Sport wanaikabili Mgambo ambayo imepoteza michezo miwili, ikiwa imeshinda mara moja na kupata sare katika gemu moja.
Mgambo ilichapwa 1-0 na Prisons imefanikiwa kufunga magoli matatu na kuruhusu nyavu zao cheza mara nne, ni timu yenye safu nzuri ya ulinzi lakini haina makali katika safu ya mashambulizi kama ilivyo kwa wapinzani wao Sport.
TANZANIA PRISONS v MWADUI FC
Kikosi kilichotazamiwa kutamba msimu huu ni cha Mwadui FC chini ya kocha, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kinaendelea ‘kusafa’ licha ya kukusanya wachezaji mastaa wenye uzoefu kama, Shaaban Kado, Paul Nonga, Razaq Khalfan, Rashid Mandawa, Nizar Khalfan, Said Sued, Malegesi Mwangwa, Jabir Aziz, Malika Ndeule, Bakari Kigodeko, Anthony Matogolo, Athumani Idd ‘Chuji’ na wengineo.
Mwadui imeshinda mara moja tu katika michezo minne iliyopita, imepoteza michezo miwili, sare imetoa mara moja Jumamosi iliyopita walipolazimisha sare-tasa dhidi ya Coastal. Prisons wameanza msimu kwa matokeo mazuri ya wastani, wameshinda gemu mbili na kupoteza mbili. Mechi hii inazikutanisha timu zilizofunga magoli mawili kila moja. Mwadui imeruhusu magoli mawili wakati Prisons imeruhusu magoli matano.
MECHI NYINGINE
Kagera Sugar v JKT Ruvu
Majimaji FC v Ndanda FC
Filed Under:
LOCAL NEWS,
SPORTS
on Wednesday, September 30, 2015
Post a Comment