Na Simon Chimbo:
Waswahili wana usemi wao usemao, ‘tonge la mwisho ndilo linalokomba mboga’… ni usemi unaojieleza sana katika maisha ya kawaida ya kila siku.
Kuna siku niliwahi kukaa na rafiki yangu mmoja mtu wa mpira mpira na hicho kikao kilikuja mara baada ya FA ya uingereza kuwapa tuzo za heshima viungo Steven Gerard na Frank Lampard mwisho wa msimu ulioisha kwa kuibariki Premier League.
Nilimuuliza swali rafiki yangu kwamba hivi ni kwanini Vodacom & TFF hawawapi tuzo za heshima Mrisho Ngassa na Juma Kaseja? kwa kuibariki ligi yetu kwa takribani muongo mmoja hivi sasa?
Kwangu mimi, Mrisho Ngassa ni moja kati ya kipaji adimu kuzaliwa nchini kwa miaka kumi iliyopita. Bila kumsahau Samatta Mbwana.
Hakuna mchezaji pamoja na mfumo usio wa kiueledi sana nje ya uwanja, angeweza kucheza katika fomu ya juu tena klabu kubwa tupu nchini za Simba, Yanga na Azam kama alivyoweza Ngassa.
Hebu tuweni makini, hii ‘consistency’ ya Mrisho sio ya kubezwa hata kidogo kwa mchezaji ambaye hata Academy anaisikia kwenye bomba.
Tangu nianze kumsikia Ngassa mwaka 2006/7 akiwa Kagera Sugar nikiwa kidato cha tatu hadi leo nina degree Mrisho hajawahi kuwa chini na ndio sababu ameendelea kuwa na thamani yake na hata ananunuliwa na timu kubwa tupu.
Jina la Ngassa huwenda ndilo linatajwa zaidi Afrika Mashariki kuliko la mchezaji yeyote kwa kipindi cha miaka 5. Anastahili pongezi kwa hilo.
Pamoja na mambo mengi nje ya uwanja lakini bado Mrisho alipata nafasi ya kucheza na Manchester United, huku pia akifanyiwa majaribio na klabu ya West Ham United ya London.
Sitaki kumlaumu Ngassa kwa kukataa ofa ya kwenda Sudan na kusaini Yanga, kwasababu Ngassa hakuwahi kufundishwa wala kushauriwa misingi muhimu ya maisha ya soka.
Lakini nawalaumu sana, tena sana Yanga ambao hata wameambulia patupu kwa usajili wa Mrisho Afrika Kusini.
Yanga wamekataa kumuuza Ngassa mara wa kadha huko nyuma, nikianzia na Norway, Sudan na kwingineko kwa sababu zisizo za kiueledi sana.
Kipaji hiki cha Ngassa kingekuwa sifuri kama leo hii ningesikia yuko Mwadui, mara baada ya kutopewa mkataba na Yanga kwa kutoamini uwezo wake (pengine Sherman ana uwezo zaidi yake).
Lakini pamoja na skendo za magazeti nje ya uwanja, mambo binafsi ya ndoa yake, kukatwa mshahara Yanga ili alipe deni na mengine, Mrisho anatakiwa amshukuru sana Mungu.
Amshukuru Mungu kwa kuwa sasa kapata mkataba mnono katika klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini, ni hatua kubwa katika career yake lakini pia neema kwa taifa letu.
Kama ni ugali, basi Ngassa hilo ndio tonge la mwisho, komba mboga sasa.
Kwa umri wa miaka 26, ndio umri wa kucheza sasa. Yaya Toure anasifika leo kuwa ni miongoni mwa viungo bora zaidi duniani lakini ana miaka zaidi ya 31.
Afrika kusini sehemu nzuri, Nonda alitokea hapo kwenda ughaibuni, hata Ngassa anaweza kufanya hivyo, ni kuvaa mkanda.
Lakini kwa mkataba huo mnono wa Free State Stars bila shaka hatutakuja kusikia miaka kadhaa ijayo kwamba, tumchangie mwenzetu kwani hana kitu, ni aibu. Wakati ndio huu wa kupiga ndege watatu kwa jiwe moja.
Safari ya Ngassa Afrika kusini inafungua njia kwa watanzania wengine kuaminiwa nje tofauti na ilivyokuwa awali, sasa Uhuru Seleman naye kapata shavu Jomo Cosmos huko huko kwa Madiba, ni neema.
Mwisho nitoe wito wa vilabu vyetu hususan ‘kulwa na Doto’ kujifunza kuwa na maamuzi sahihi na hasa ya kuwasaidia wachezaji wetu.
Leo hii Yanga wangemuuza Mrisho, kwanza wangepata sifa, pesa na wachezaji wengi wangekimbilia kwao kwa kuamini kumbe ni njia ya kutokea.
Tusiwabane wachezaji wanapopata fursa nje. Kama Yanga/Simba wangekuwa ndio Manchester United, basi wasingemuuza Cristiano Ronaldo wakati ule kwenda Madrid.
Nakutakia kila la kheri Mrisho, uko katika kipindi muhimu mno cha safari ya maisha yako ya soka, usibweteke.
chimbo445@gmail.com
KUJIUNGA NA KINYANG'ANYIRO CHA PIKIPIKI AINA YA BOXER BONYEZA PICHA CHINI YA MANENO HAYA NA UIBUKE MSHINDI,BONYEZA MARA NYINGI UWEZAVYO KUIBUKA MSHINDI;
Post a Comment